Jumuiya ya Wazanzibari Waishio Tanganyika imekuja juu ikipinga vikali
mikakati ya kuwabagua inayolenga kuwatisha ili kuwarudisha nyuma
wasiendelee kudai mamlaka kamili ya Zanzibar pamoja na Muungano wa haki
na wenye maslahi kwa pande zote mbili.
Mikakati hiyo inadaiwa kufanywa na watu wa kubuni wanaojiita Umoja
wa Wapemba Waishio Tanzania Bara (Neppelta) kwa kutumia hotuba ya Rais
Jakaya Kikwete, aliyoitoa wakati akizindua Bunge Maalumu la Katiba,
Machi 21, mwaka huu.
Tamko la jumuiya hiyo lilitolewa na Mwenyekiti wake, Abdallah Mohammed Kassim, marufu kama “Dullah”, jijini Dar es Salaam juzi.
Alisema kauli ya watu hao, ambayo ilinukuliwa na baadhi ya vyombo
vya habari hivi karibuni, imeonyesha ubaguzi wa dhahiri dhidi ya
Wazanzibari, ambao kiasili ni wamoja licha ya kutenganishwa na bahari.
Abdallah alisema hawakubaliani na kauli ya watu hao iliyosisitiza
kuwa wao ni “Wapemba” kwa kuwa Zanzibar ni moja na maslahi yake ni ya
wote.
“Kitendo cha kusisitiza kuwa Muungano ukivunjika watakaopata hasara
ni Wapemba ni ubaguzi kwani Wapemba ni Wazanzibar hivyo kuwabagua ni
kujenga chuki miongoni mwa raia wa visiwa hivyo viwili ambao ni wananchi
wa nchi moja,” alisema Abdallah.
Alisema Muungano uliopo ni wa nchi mbili, ambazo ni Tanganyika na
Zanzibar na kwamba, Zanzibar ni visiwa vya Unguja na Pemba, hivyo
kuendelea kuwabagua Wapemba kwa maneno na vitendo ni kutowatendea haki.
Abdallah alisema uamuzi wa Wazanzibari kuishi na kufanya kazi
Tanganyika ni haki yao ya msingi, hivyo kuwajengea hofu ni kuwanyima
haki hiyo na kuwafanya waishi kwa mashaka makubwa, kitu ambacho alisema
siyo kizuri kwa raia.
“Jumuiya ya Wazanzibari tunaoishi Tanganyika tunauliza kauli
iliyotolewa na bwana Shehe Haji Faki ambaye alijitambulisha kama
Mwenyekiti wa Wapemba waishio Bara kwa kusema idadi ya Wapemba waishio
Bara imeongezeka hadi kufikia zaidi ya watu 800,000 mwaka 2012 na mtaji
wa trilioni 1.2, takwimu hizi amezipata wapi?” alihoji Abdallah.
Alisema uhusiano na mwingiliano baina ya Wazanzibari na Watanganyika vilikuwapo kabla ya Muungano wa mwaka 1964.
Hivyo, akasema kuishi katika nchi yoyote duniani hakutegemei
Muungano, kwani wapo Watanzania wanaishi nchi mbalimbali duniani bila
ubaguzi na hata Tanzania wapo raia wengi wa kigeni wanaoishi licha ya
kuwa nchi hizo hawajaungana nazo.
“Wazanzibari waliopo Tanganyika na kumiliki ardhi na mali isiwe
sababu ya kuwatisha na kuwajengea hofu ya kudai maslahi ya nchi yao,
kwani utaifa wa mtu hauwezi kutupwa kwa sababu ya kumiliki ardhi, mali,
kuoa au kuolewa,” alisema Abdallah.
Alisema umoja uliopo miongoni mwa Watanzania unakumbusha kuwa
wanaofaidika na Muungano siyo Wazanzibari pekee, kwani faida hizo zipo
kwa raia wa pande zote mbili za Muungano.
CHANZO: NIPASHE
Home
Unlabelled
Wazanzibari waishio Tanganyika wapinga kugawanywa
Wazanzibari waishio Tanganyika wapinga kugawanywa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment