
HUKU Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiwa kimeweka bayana kwamba
hakiungi mkono Serikali tatu kama Rasimu ya Katiba inavyoonyesha, Waziri
wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ameibuka na kusema endapo Mabaraza
ya Katiba yatawasilisha hoja za kuikubali, kuna uwezekano mkubwa wa
Uchaguzi Mkuu wa 2015 kukwama.
“Uwepo wa Serikali tatu utafumua mfumo mzima wa
utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya uchaguzi wa Rais na
wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya Serikali Tatu
kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na Serikali
tatu.
“Kama tutafanya uchaguzi, utafanyika kwa taratibu
zipi, ipi itakuwa mipaka ya marais wa Serikali tatu, makamu na mawaziri
wakuu, mfumo wa Mahakama, Tume ya Uchaguzi, utendaji wa Bunge na
wabunge, yako mengi, sasa mpaka hayo yaingie kwenye Katiba,” alisema
Chikawe juzi Dar es Salaam.
Alisema lazima CCM isimamie suala hilo kwa kuwa
kukubali Serikali tatu kutaua Muungano ambao sehemu kubwa unalindwa na
chama hicho tawala.
“CCM wamejipanga kama baraza na kusimamia hili la
Serikali mbili ambalo lengo ni kuulinda Muungano. Litakapokuja hili la
Serikali tatu, lazima Muungano uparaganyike,” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Waziri Chikawe
inakinzana na ile aliyoitoa Juni 4, siku moja baada ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba kutangaza hadharani Rasimu hiyo.
Waziri huyo alikaririwa na gazeti hili akisema upo
uwezekazo wa Katiba Mpya ya Tanzania Bara ikapatikana kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015 ikiwa mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano
utakamilika kama inavyokusudiwa na rasimu hiyo kupitishwa na wananchi
katika ngazi zote bila mabadiliko.
“Watu wasiwe na hofu. Sioni tatizo endapo rasimu
itapita bila mabadiliko na kupata Katiba Mpya. Aprili mwakani mpaka
Desemba inatosha kabisa kuandaa Katiba ya Tanzania Bara na tukaenda
katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na Katiba Mpya,”alikaririwa akisema na
kuongeza:
“Tunaweza kuwatumia wajumbe walewale wa Tume ya
Katiba lakini safari hii tukawachukua wale wa Tanzania Bara pekee
wakashiriki katika kuandaa Katiba hiyo.”
Alisema kutokana na muda kuwa mfupi, Tume hiyo
inaweza isifanye kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kama
ilivyofanya sasa na badala yake ikaandaa rasimu na kujadiliwa na wadau
kisha kupelekwa katika mabaraza ya Katiba kabla ya kupata Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa
kukamilika Aprili mwakani.
Alisema kuanzia hapo, Serikali inaweza kuitumia
tume ya sasa kutangaza rasimu ya kwanza ya Katiba ya Tanzania Bara kwa
kurejea maoni iliyokusanya hivyo hatua ya kwanza ikawa ni kujadiliwa kwa
rasimu hiyo kwenye mabaraza ya Katiba kwa miezi miwili na baadaye
kupelekwa katika Bunge la Katiba jambo litakaloifanya ipatikane mapema.