Kundi
la wazazi wa watoto wanaosoma katika Shule ya Msingi Kinole, iliyopo
katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro, wamevamia
shule hiyo na kuwachapa walimu bakora na kusababisha baadhi yao (walimu)
kujeruhiwa.
Habari
kutoka shuleni hapo zilizothibitishwa na Ofisa Elimu wa Halmashauri
hiyo, Donald Temba, zinaeleza kuwa wazazi hao walifanya kitendo hicho
juzi wakidai kuchoshwa na vitendo vya walimu hao vya kuwachapa watoto
wao.
Kutokana na tukio hilo, uongozi wa halmashauri umeifunga shule hiyo hadi hapo maamuzi mengine yatakapotolewa.
Akielezea tukio hilo, Temba alisema lilifanywa na wazazi hao baada ya walimu kutoa adhabu kwa wanafunzi kwa makosa waliyofanya.
Alisema wazazi hao walivamia shule hiyo wakimtuhumu Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Jaka Lukome, kuwachapa wanafunzi wawili bakora.
Kwa mujibu wa Temba, wanafunzi hao walichapwa bakora siku mbili zilizopita kutokana na kosa la kupigana wakiwa shuleni.
“Kuna adhabu zilikuwa
zimetolewa kwa wanafunzi wawili wa shule hiyo. Ndiyo kikawa chanzo cha
wazazi hao kuandamana na kuvamia shuleni hapo na kuwapiga bakora
walimu,” alisema Temba.
Hata hivyo, alilaani kitendo cha wazazi kuvamia shule na kuwachapa walimu bakora.
Alisema kitendo hicho kinaweza
kuzorotesha maendeleo ya elimu katika kijiji cha Kinole kutokana na
walimu kuogopa kufanya kazi katika shule hiyo.
Aliutaka uongozi wa serikali
ya wilaya ya Morogoro kuwachukulia hatua za kisheria wazazi waliofanya
kitendo hicho kwa kuwa kimewadhalilisha walimu mbele ya wanafunzi wa
shule hiyo.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya hiyo, Julius Madega, alisema wamefikia hatua ya kuifunga
shule hiyo baada ya kutokea vurugu hizo na hivyo kuhatarisha amani dhidi
ya wazazi na walimu.
Alisema wanakusudia kuwahamisha baadhi ya walimu na kuwapeleka shule nyingine, akiwamo mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Nao wakazi wa wilaya hiyo, Gladness Masimba na Abdallah Mwombosa, walilaani kitendo cha wazazi hao kuwachapa walimu bakora.
Walisema kitendo hicho ni kibaya kwani kitachangia kuua elimu katika kijiji hicho.
Waliutaka uongozi wa wilaya
kuwachukulia hatua kali wazazi hao ili kukomesha tabia hiyo kwa wengine
wanaofikiria kufanya kitendo hicho.
Hata hivyo, kufuatia vurugu
hizo Jeshi la Polisi Wilaya hiyo ya Morogoro inawashikilia wahusika wa
tukio hilo na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
Swahili TZ.